Kufanya kazi na watu wanaoishi na ugonjwa
Hakuna njia moja ya kujumuisha watu wanaoishi na ugonjwa wa dementia katika kazi yako. Kuhusisha watu walio na ugonjwa wa dementia na familia zao ni jambo la kimsingi katika kazi ya kupinga unyanyapaa: Tunahitaji kuelewa nini cha dhamana sana kwa watu wanaoishi na ugonjwa wa dementia na maono yao na matumaini ya mabadiliko ya jamii ili kuwa na athari ya maana. Hii inamaanisha kuelewa mambo ambayo wamepitia ya kutotendewa haki na matendo na tabia ambazo ni za kuumiza zaidi.
Pia, tunahitaji habari kuhusu ni matendo yapi yanayowezesha zaidi na ni raslimali gani na msaada upi unaohitajika ili kukabili unyanyapaa na kuishi maisha bora. Kwa hivyo, ni muhimu watu wanaoishi na ugonjwa wa dementia kuwa katikati ya kazi ili kuhakikisha mpango una maana kwao.
Maono ya jinsi ya kupunguza unyanyapaa na kuwezesha watu wanaoishi na ugonjwa wa dementia yanatofautiana kulingana na tamaduni na mahali. Kwa hivyo, hatuwezi kutoa njia moja ambayo ni bora kwa kila mtu ya kufanya kazi hii. Badala yake, tunatoa kanuni na mapendekezo ya kufanya kazi kwa pamoja na watu wanaoishi na ugonjwa huu, kuhakikisha kuwa watu wanaoishi na ugonjwa wa dementia wako na umuhimu zaidi kwa maono ya mpango wakupinga unyanyapaa na shughuli hizi.
1 Kazi na fursa zinafaa kuwa wazi kwa kila mtu.
Watu wanaoishi na ugonjwa wa dementia ni kikundi chenye utofauti. Katika kupunguza unyanyapaa, ni muhimu kukumbuka kuwa shughuli na fursa zinafaa kuwa wazi kwa kila mtu. Baadhi ya watu wanaweza kupata vikwazo zaidi katika kuhusika. Mara nyingine hii ni kutokana na kiwango cha ugonjwa wa dementia, ila kutofikiwa pia kunaweza kutokana na jinsia, kabila, kikundi cha kiuchumi na kijamii, mwelekeo wa ngono, masomo, umri au mambo mengine.
Wakati unapoanza mpango mpya wa kupinga unyanyapaa, ni kawaida kwa viwango vya kuhusika kuwa ndogo mwanzoni. Kama hakujakuwa na shughuli nyingi katika jamii, kunawezekana kuwa tu na idadi chache ya watu ambao wamezungumzia hali yao awali. Pia, inaweza kuwa sio kawaida kuzungumzia hadharani kuhusu hali ya mtu, na hivyo tunapaswa kushukuru watu wa kwanza wanaojitokeza kuzungumzia mambo yao.
Hata hivyo tunafaa kujua tokea mwanzo vikundi tofauti ambavyo vinaathirika na dementia wakati wa kuanzisha mpango wowote na kuwa na mpango na mwongozo wa kusajili watu tofauti na kupata maoni tofauti, hata kama hii itatokea baadaye katika mpango. Hii inaweza, kwa mfano, kuhitaji kuelewa vikwazo vya kuhusika kwa vikundi tofauti na kuzungumza jinsi ya kushinda vikwazo hivi.
2 Tambua kuwa fursa za utetezi kwa watu wanaoishi na dementia na watunzaji wao zinaweza kuwa za aina tofauti
Utetezi kwa watu wanaoishi na dementia sio tu kuhusu kuzungumza hadharani. Hivyo, ni muhimu kutoa fursa mbali mbali. Kuhusika kunaweza kuboreshwa kwa kukubali na kusaidia watu wanaoishi na ugonjwa wa dementia wenye uwezo na mapendeleo tofauti. Kwa mfano, watu walio na matatizo ya lugha wanaweza kubali kazi ya sanaa na njia zingine za kuona ili kushiriki ujumbe wao na wengine wanaweza pendelea kutumia ushairi, muziki ili kupeana ujumbe wao wakiwa peke yao au kwa kikundi, au kwa msaada wa, kwa mfano watunzaji wao.
3 Kuzungumzia mambo mtu amepitia katika kuishi na ugonjwa wa dementia ni chaguo la kibinafsi
Tunahitaji watu jasiri kujitokeza na kuzungumzia hadithi zao za kuishi na ugonjwa wa dementia ili kupigana na unyanyapaa vyema. Kwa kweli, kushiriki habari ya mtu kunaweza kusaidia watu kuhisi kupumzika kwa sababu hawahitaji kuishi kwa siri tena. Hakuna aibu kuishi na ugonjwa wa dementia, hata hivyo inafaa bado kuwa chaguo la mtu kushiriki habari zake au la. Hivyo, watu walio na ugonjwa wa dementia wanafaa kudhibiti iwapo washiriki mambo ambayo wamepitia, kwa nia gani, kwa nani, na aina ya habari za kina wanataka kuweka wazi. Gharama na faida za kueleza habari ya mtu zinaweza kuwa tofauti kulingana na mahali mtu anaishi, nani wanazungumzia na habari wanazotoa. Watu wanaweza penda kushiriki habari zao kwa njia tofauti. Watu wengine wanaweza kuwa hawako tayari kushiriki kwa uwazi na wangependa kushiriki bila kutambulika.
4 Saidia watu kubaini gharama na faida ambazo zinaweza kuwemo katika kuzungumzia mambo ambayo wamepitia ya dementia na kutoa msaada na ulinzi kwa wale wanajitokeza
Kwa kweli, mipango ya kupinga unyanyapaa inajaribu kujenga utamaduni ambao ni wazi na wa msaada kwa watu wanaoishi na ugonjwa wa dementia ili wasiwe na athari mbaya kutokana na kuelezea ugonjwa wao. Kueleza habari ya mtu ya kibinafsi ya mambo ambayo amepitia katika jamii iliyo na ufahamu haba na msaada duni kwa watu wanaoishi na dementia, au ambapo ni kawaida kuwatenga watu wanaoishi na ugonjwa wa dementia, kunaweza kuwa na hatari.
Waanzilishi ambao wanaongoza harakati mara nyingi huitaji ujasiri kwa wingi ili kuleta mabadiliko ya jamii. Hivyo, ni bora kusaidia watu wanaojitokeza kutathmini gharama na faida za kushiriki habari zao hadharani na kuwaza kuhusu jinsi wanaweza kufanya hivi kwa njia salama ambapo wanahisi kuridhika.
Watu wengi wanaoshiriki habari yao pia wanaashiria faida pamoja na kukutana na wenzao (wanaoishi na ugonjwa wa dementia na watunzaji wao) pamoja na kupunguza unyanyapaa na aibu ya ndani.
Hii inamaanisha kuunda fomu za kutoa idhini zenye zinarejelewa kwa pamoja kwa makini na ambazo zinaeleza maswala haya kwa njia iliyo wazi na inayoeleweka. Pia, ni muhimu kutambua aina tofauti za msaada zilizopo. Hizi ni pamoja na mashirika ya eneo na raslimali za mtandao lakini pia unafaa kutambua mtu mmoja kwa jina kutoka kwa kikundi ambaye unaweza wasiliana naye iwapo patahitajika masaada.
Habari hii inafaa kupeanwa mwanzoni. Pamoja na kupeana habari hii ni muhimu kuwasiliana na watu wa kujua jinsi wanavyoendelea na kuhakikisha wako salama na hawako kwa hatari.
5 Fursa za kuunda ujuzi na uzoefu
Watu wanaoishi na ugonjwa wa dementia wanaweza kuwa na uwezo tofauti, maadili na malengo ambayo wanataka kuafikia na kuchangia katika mpango wa kupunguza unyanyapaa. Kwa hivyo, ni muhimu kufanya kazi kwa pamoja na watu wanaoishi na ugonjwa wa dementia kutathmini kiwango cha kuhusika ambacho wanataka na ni wapi wanataka kuzingatia.
Watu wengine wanaweza kupendelea kuwa na nafasi ya kisiri na wengine wakawa radhi na mazoea ya kuzungumza na kwa hivyo kuwa na nafasi ya kutumika hadharani. Hata hivyo, baadhi ya watu wanawezataka kushiriki hadithi yao hadharani, ila wanahitaji msaada ili kufikia lengo hili. Kutoa mafunzo na msaada kunaweza hitajika katika jambo hili ili waweze kufanya kazi na kuhusika kwa wingi.
Mpango unapaswa kulenga kuwawezesha na kuwasaidia watu kufikia malengo yao katika mradi wa kupinga unyanyapaa na kutambua fursa zifaazo, mafunzo na msaada ili kusaidia watu kuhusika.
6 Kupata vifaa vya utetezi
Ni muhimu kukua na ufikiaji wa vifaa kwa upana unaofikia watu tofauti. Ingawa unyanyapaa ni swala la kote ulimwenguni, vifaa vingi vya utetezi vinapatikana kwa lugha ya kiingereza tu na zinatoka nchi zenye mapato ya juu.
Hii ni licha ya ukweli kua 70% ya watu wanaoishi na ugonjwa wa dementia wanaishi katika nchi zenye mapato ya chini na ya kati. Kutafsiriwa kwa lugha zingine kunaweza kusaidia kufikia watu wengi zaidi.
Pia, ingawa unyanyapaa kwa njia moja ni jambo linalopatikana kote ulimwenguni, tofauti katika mambo ambayo watu wanapitia ya kutengwa yanaweza kutokana na tofauti za kijamii, kitamaduni na kisiasa na kugeuzwa kufikia tamaduni za eneo na kuwekwa katika eneo kunaweza kusaidia kufanya ujumbe na vifaa kuwa za kufana na kukubalika katika mazingira tofauti.
Muungano wa eneo wa Alzheimer's na dementia ni mahala ambapo vifaa hivi vinaweza kupatikana. Mshirika wetu Alzheimer's Disease International anatoa habari kuhusu mashirika ya eneo (www.alzint.org)
7 Fidia watu kwa muda na utaalamu wao
Kama tulivyojadiliana, kuhusisha watu wanaoishi na ugonjwa wa dementia ni msingi kwa mpango wowote wa kupinga unyanyapaa, na hivyo wakati unapanga shughuli, ni muhimu kuwaza jinsi ya kuthamini mchango wao.
Hii inajumuisha kupanga awali aina ya shughuli ambazo zitatekelezwa na jinsi shughuli hizi zinalingana na raslimali zilizopo. Pia, inamaanisha kubuni mwongozo wa jinsi ya kukumbana na malipo pamoja na kulipwa kwa mchango wao (pamoja na kiwango cha malipo na jinsi yatatolewa), kufidia gharama zao na jinsi kuhusika kwao kutatambuliwa.
Mara nyingine, pia inafaa kutoa faida nyingine kama mafunzo, fursa za kijamii, shahada, fursa ya kuzungumza na kushiriki masomo ya mpango. Michakato hii ya fidia inafaa kuelezwa kwa uwazi kwa wale wanawaza kushiriki.
Pia, maana ya uzoefu na ujuzi wa watu wanaoishi na ugonjwa wa dementia na watunzaji wao inafaa kuelezwa wazi kwa wale wanaohusika katika kupeana mipango ya kupinga unyanyapaa mwanzoni na kila wakati katika mpango.